The Love Blog

Lazima uwe makini wakati wa kutafuta mke!

Tunaangalia umakini wakati wa kumtafuta mke mwema, ni wiki ya nne sasa tunaangalia sifa za mwanamke anayefaa kuwa mke. Kimsingi sio kila mwanamke anafaa kuwa mke! Unaweza kuwa mwanamke, lakini usiwe mke! Hii ndio sababu nachambua mada mbalimbali za kuweza kupata wenzi sahihi wa maisha. 

Katika mada hii, bila shaka wanaume wanapata nafasi ya kuweza kuwatambua wenzi sahihi wa maisha, lakini pia wanawake wanapata nafasi ya kutoka katika sehemu waliyopo ambayo napenda kuiita gizani na kurudi kwenye nuru ili waweze kupata wenzi wa maisha yao.

Hebu sasa tuendelee na vipengele vinavyofuata…

ANAYEJALI USAFI!
Kama ni mchafu atakuwa mwanamke wa aina gani? Maana tumezoea kusikia kila wakati kuwa mwanamke ni pambo la nyumba, sasa atawezaje kuwa pambo la nyumba wakati ni mchafu? Hili sio suala la kufundishana, ni hulka ya mtu ambayo huzaliwa nayo.

Jaribu kuvuta picha, umetoka kazini ukiwa umeongozana na rafiki zako. Kwa mbwembwe zote unataka kuwakaribisha nyumbani kwako. 

Unafika unamkuta mtoto kajisaidia haja kubwa mlangoni, tena anachezea kinyesi chake mwenyewe, mkeo hana habari kabisa, amekaa kwenye jamvi yupo bize anapiga soga na shoga zake, akiwa mchafu! Atakuwa mke kweli huyo au matatizo?

Sifa ya mwanamke ambayo karibu wote hupaswa kuwa nayo, ni pamoja na usafi. Usafi ni kitambulisho cha mwanamke. 
Kama asipokuwa msafi, ni rahisi familia yako kushambuliwa na magonjwa ya mlipuko. Ni lazima mkeo awe msafi.

ANAKUHESHIMU...
Hili sio ombi, ni amri! Mwanamke anapaswa kumheshimu mumewe, sasa dalili za heshima huanza kuonekana tangu mapema wakati wa uchumba. 

Kama upo katika uhusiano na mwanamke ambaye hana heshima, ni dalili za kupata mke asiye na heshima. Tabia hii nayo haibadilishiki, ni lazima uwe makini sana na mwanamke wa aina hii.

Dalili ya kwanza ambayo unaweza ukaiona ni kutojali unayomwambia, mathalani unamzuia kuvaa nguo ya aina fulani halafu analazimisha kuvaa, hilo ni tatizo na usitegemee atabadilika mkiwa ndani ya ndoa. Atakuwa tatizo zaidi na zaidi! Sasa usikubali kufuga matatizo. 

ANAJALI NASABA YAKO!
Ili awe mke kamili atakayefaa ndani ya nyumba lazima awe na sifa hii! Asiishie kusema kuwa anakupenda wewe lakini ndugu zako anawadharau, hayo sio mapenzi. Lazima aonyeshe kukujali wewe na ndugu pamoja na jamaa zako, hayo ndio mapenzi ya dhati yanayopaswa kuwa nayo mwanamke mwema.

Hilo linaweza kuonekana kuanzia siku utakayomtambulisha kwa rafiki zako wa karibu. Kama ni kweli anakupenda na ana nia ya kuishi na wewe katika maisha yake yote, atakubali kuwa na ndugu zako, kushirikiana nao kwa kila kitu, na kuwajali kama wewe!

Ukimwambia akae na mama yako kwa kuwa ni mgonjwa hapaswi kukataa, akifanya hivyo ujue kuna tatizo hapo! Kama hatampenda mama yako ambaye amekuleta duniani, atampenda nani zaidi? Pambanua mwenyewe!

USIKUBALI KUSHINIKIZWA!
Pamoja na yote niliyoandika lakini hivi sasa kuna tabia moja ambayo sio nzuri, iliyopo kwa baadhi ya jamii yetu, kushinikiza! Kamwe usikubali kuishi na mwanamke ambaye unaamini huna mapenzi naye. 

Kama wazazi wako wanalazimisha jambo hilo, ni vizuri ukakaa na kuzungumza nao kwa undani na uwaeleze athari za kuishi na mwanamke ambaye hujampenda.

Hili ni rahisi kidogo, kwa kuwa unaweza ukazungumza na wazee ambao wataweza kufikisha ujumbe huu kwa wazazi wako. Kuishi na mwanamke usiyempenda ni matatizo, unaweza ukajikuta ukimfanyia vituko mtoto wa watu bure! Zungumza na wazazi wako!

ANGALIZO KWA WANAWAKE
Wewe msichana unayesoma mada hii unapaswa kubadilika! Wanaume waoaji siku hizi ni wachache sana. Kumbuka kuwa mwanamke anapoolewa ni heshima kwake na familia nzima kwa ujumla, lilia heshima hiyo, usikubali kuishi bila heshima hii. Lakini ili uweze kuipata lazima uwe na sifa nilizozianisha kwa majuma manne mfululizo.

Kama ni kweli unataka kuingia kwenye ndoa, anza kufanya mabadiliko katika mienendo yako kuanzia leo. Jenga heshima katika maisha yako yajayo, anza kutengeneza njia za kuonwa mwanamke bora!

Followers