The Love Blog

Akiwa na sifa hizi ruksa kumuoa


Naomba kuchukua nafasi hii kuwakumbusha wasomaji wangu wapenzi kwamba kitabu changu cha True Love (Penzi la Dhati) kinapatikana mitaani kwa wauza magazeti wote. Ni kitabu chenye mada nzuri za mapenzi, pamoja na love sms (ujumbe wa mahaba) kali kwa ajili ya kumtumia yule unayempenda! Baada ya hayo, sasa tunageukia mada yetu ya leo, nazungumzia kuhusu sifa za mwanamke anayefaa kuwa mke bora.

Katika mambo muhimu ambayo unapaswa kuelekeza akili yako yote katika kufanya maamuzi ni pamoja na mapenzi! Ukioa mwanamke ambaye unadhani unampenda au ukaolewa na mwanaume ambaye unadhani unampenda kumbe sio hivyo, au baada ya kuingia katika ndoa ukakutana na mambo mengine ambayo hukuyategemea, uwezekano wa kuharibu maisha yako na kuona mapenzi machungu huwa mkubwa sana!

Katika kufanya uchaguzi wa mwenzi wa maisha ni lazima uwe makini sana. Sasa linapokuja suala la kuwa na mke mwema, ni lazima ujue sifa anazotakiwa kuwa nazo. Kama unataka kuoa lazima mwanamke huyo awe na sifa zifuatazo:

HANA TAMAA...
Mwanamke anayefaa kuolewa ni lazima asiwe na tamaa, awe anaridhika na kile kidogo anachopewa na mpenzi wake. Kutamani kila kitu au kutaka vitu vikubwa ni tatizo kubwa sana katika ndoa. Ikiwa upo katika uhusiano na mwanamke mwenye tamaa, anza kujiuliza mara mbili.

Mchunguze vizuri utakuja kugundua nia yake ni kukuchuna tu na sio kuishi na wewe katika ndoa. Huo ndiyo ukweli ambao upo hata kama utakuumiza.

HAEHESABU MAKOSA
Hii ni kati ya sifa za mwanandoa bora, ili uwe mwanandoa kamili lazima uwe na ‘kifua’, sio kila kitu unanung’unika na kuanika nje! Kuanzia mnapokuwa marafiki, anza kumchunguza mchumba wako, ukimkosea na kumuomba msamaha, akishakusamehe hurudia tena kukuuliza? Ukiona anafanya hivyo, tambua kuwa huyo sio mke bora.

Mwanamke mwema siku zote huangalia mbele, sio ukifanya kitu kidogo tu, anaanza kukuuliza juu ya makosa yako ya nyuma; “Kila siku unaomba msamaha, wewe ni mwanaume wa aina gani? Mara ya kwanza uliniomba msamaha nikakubali, ukarudia tena nikakubali leo tena, ah nimechoka!” Haya ni baadhi ya maneno ambayo hutumiwa na wanawake wa aina ninayoizungumzia katika mada hii. 

MOYO WAKO URIDHIE!
Hii isibaki kuwa hadithi za kufikirika, iwe yakini na moyo wako uzungumze hivyo, kuwa unampenda kwa mapenzi ya dhati! Utajuaje kama unampenda? Sema na moyo wako utakupa ukweli juu ya hilo, usikurupukie mapenzi, usije ukamuona msichana siku moja amevaa suruali inambana kiasi cha kuonyesha umbile lake halafu ukamtamani ukadhani unampenda, utakuwa unapotoka!

Mapenzi sio kitu cha mchezo, huanza moyoni jiridhishe kwanza ndipo ukubali kumwingiza katika moyo wako. Kumbuka kitu kimoja, unapoamua kufunga ndoa na mtu ni ahadi ambayo mmeahidiana mbinguni na duniani, ni ahadi ambayo inapaswa kutenganishwa na kifo tu, sio vinginevyo! Kamwe usifanye majaribio katika mapenzi, mapenzi hayajaribiwi!

NI KWELI ANAKUPENDA?
Hili ni muhimu kuliko la kwanza, ingawa ni vizuri kuishi na mwanamke unayempenda lakini pia ni lazima awe anakupenda! Sio vigumu sana kumfahamu mwanamke anayekupenda, lakini pia inawezekana ukaona anakupenda kumbe ni danganya toto!

Kimsingi katika hili ni lazima utumie akili yako yote uweze kutambua hilo. Mwanamke anayekupenda huwa mvumilivu, anayekusikiliza pia mwenye kuwajali ndugu, marafiki na jamaa zako! Hii ni alama nzuri ya kuwa na mke mwema anayekubalika na ndugu zako pamoja na rafiki zako wa karibu.

MWEREVU...
Siyo lazima awe na elimu ya darasani, haijalishi ni mwanamke aliyekulia kijijini au mjini, lakini hapa tunaangalia uwezo wake wa kufikiri, ni mwerevu? Anayejua mambo na njia za kuyatatua? Hili ni jambo la msingi sana kulifahamu.
Hata hivyo, inategemea wewe umepanga kuishi na mwanamke wa aina gani, lakini mwanamke ninayemzungumzia hapa ni yule mwenye uwezo wa kutosha wa kufikiri na kupambanua mambo!

Mwenye uwezo huu ni yule ambaye ukimwambia kuwa kibanda chako unachofanyia biashara Kariakoo kimevunjwa na Askari wa Jiji, atakuwa na ushauri wa kukupa utakaokusaidia kuendesha maisha yako na sio kukulaumu au kuishia kukusikitikia bila kuwa na wazo la kukupa. Kusikitika kwake hakumaanishi kuwa yupo pamoja na wewe, atakuwa pamoja na wewe pale atakapoonyesha njia nyingine ya kukusaidia kujikwamua kimaisha.

Sio kuishia mizinga kila siku, mara simu haina dola, mara mama Juma amepitisha vitenge anakopesha, lazima uangalie je, unapokwama anakuwa pamoja na wewe kifikra au ni mzigo wa mananasi? Hilo ni la kuzingatia sana katika maisha ya sasa.

Mwanamke wa aina hii unapaswa kumchunguza mapema ili usije ukaoa mzigo! Suala la uwezo wa kufikiri lina umuhimu mkubwa sana katika maisha ya sasa, ni bora mkakosa mali lakini mkawa na uwezo wa kufikiri na kutatua matatizo mbalimbali ya kimaisha. Huu ndio ukweli ingawa wengi wanaukwepa! Nawasilisha.

Followers