JE, UPO TAYARI KUWA MWANANDOA? Utayari ninaozungumzia hapa ni ule wa kujiandaa kikamilifu kisaikolojia na kukubaliana na hali hiyo ya kuwa ndani ya ndoa. Mwingine anaweza akaingia katika ndoa kwa sababu fulani naye yupo katika ndoa, au akaamua kuingia katika ndoa kwa sababu ya shinikizo la wazazi, haitakiwi hivyo, ni lazima uhakikishe wewe mwenywe upo tayari kuingia katika ndoa. Usiingie katika ndoa kwa sababu una kazi, au umepata mafanikio fulani kimaisha! Hili linawasumbua wengi sana, baadhi ya vijana huingia katika ndoa baada ya kupata mafanikio katika maisha, wengi wao jambo la kwanza kuanza kulifikiria huwa ni kuoa, hili ni kosa, kwa kuwa utakuwa umeamua kuoa kwa sababu una pesa au mafanikio kimaisha lakini hukuwa umejipanga kikamilifu kwa ajili ya kuoa hasa kama hukuwa na mchumba hapo awali. “Mimi sasa hivi mambo yangu yangu safi, hakuna jambo lingine la kufanya zaidi ya kuoa! Kama ni pesa ninayo, nyumba ninayo sasa nioe ili nitulie," kauli kama hii ni ya kawaida sana kwa baadhi ya vijana wenye fikra hii potofu. Pamoja na vijana kuwa na fikra hiyo, hebu angalia na wazazi wanavyokuwa na yao vichwani mwao; "Mwanetu sasa anajiweza kimaisha ni bora sasa akaoa, akioa atatulia na kujiepusha na umalaya!" Wazazi nao husema hayo. Kimsingi ni kwamba suala la ndoa sio jambo dogo ambalo unaweza ukaamua haraka haraka bila kuwa na maandalizi ya kutosha kiali kabla. Unaweza ukajikuta umeoa mwanamke ambaye sio chaguo lako baada ya kuwa na pesa, lakini ukiingia ndani ya ndoa unakuta kumbe hakuwa mwanamke sahihi wa maisha yako. Unaweza ukapanga mambo yako kikamilifu kwanza kabla ya kuamua kuoa, usioe kwa sababu una pesa oa kwa sababu upo tayari kuingia katika ndoa. Bila shaka tayari umeshaelewa, mambo ya kuzingatia kabla ya kuingia katika ndoa. Usikurupukie ndoa kabla ya kufanya uchunguzi wa kutosha. |
The Love Blog